Agizo
la Rais John Magufuli la kusitisha safari za nje linakabiliwa na ugumu
katika utekelezaji wake kutokana na nchi kuwa na balozi 36 tu ambazo
zitatakiwa kufanya kazi maeneo mbalimbali duniani.
Muda mfupi baada
ya kuapishwa na kuanza utekelezaji wa majukumu yake ya mkuu wa nchi,
Rais alifuta safari zote za nje kwa watumishi wa Serikali na viongozi
ili kuokoa fedha zinazotumika kwa ajili hiyo na kuagiza shughuli hizo
zifanywe na mabalozi.
Rais alisema safari hizo zitadhibitiwa na
Ikulu ambayo itatoa kibali kwa safari maalumu, ikiwa ni pamoja na kuweka
masharti ambayo mtumishi anayetakiwa kusafiri atatakiwa kuyatimiza
kabla ya kupewa kibali.
Lakini utekelezaji wa agizo hilo
unakabiliwa na vikwazo vingi, hasa vikubwa vitano ambavyo ni uchache wa
balozi za Tanzania nje ya nchi, ukomo wa madaraka ya mabalozi, wigo wa
ufahamu wa mambo ya kitaalamu na ukosekana kwa mazungumzo endelevu iwapo
suala moja litawakilishwa na watu wawili tofauti kwenye mikutano miwili
tofauti.
Takwimu za Umoja wa Mataifa (UN), zinaonyesha kuwa hadi
sasa chombo hicho kina wanachama 193 ambao nchi zinazaweza kuwa na
uhusiano nazo wa kidiplomasia, kwa mujibu wa makubaliano ya wanachama wa
umoja huo. Kwa mujibu wa wakosoaji, uchache huo utasababisha mabalozi
hao kusafiri sehemu mbalimbali duniani kushiriki kwenye shughuli ambazo
viongozi wa umma walitakiwa kwenda, hali ambayo itasababisha safari
kuwapo kama kawaida isipokuwa wanaosafiri ndiyo watakaobadilika.
“Ni
kweli kwamba idadi ya watu wanaosafiri itapungua, lakini ile dhana ya
safari itabakia vilevile,” alisema mmoja wa wakosoaji ambaye hakutaka
jina lake litajwe.
“Kwa mfano, mkutano wa Jumuiya ya Madola
unaofanyika Malta, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza ndiye atatakiwa
kwenda. Kwa hiyo ni safari pia.”
Bara zima la Amerika Kusini lina
ofisi moja tu ya ubalozi iliyoko Brasilia, Brazil, wakati bara la
Amerika Kaskazini lina balozi tatu, mbili zikiwa Marekani--Umoja wa
Mataifa jijini New York na Washington--, huku Ulaya yenye nchi 50 ikiwa
na balozi nane, wakati Asia, Arabuni pamoja na Australia kuna ofisi nane
za ubalozi.
Bara la Afrika lenye nchi 52, ndiko kuna balozi nyingi zaidi, kukiwa na ofisi 14.
Ugumu
katika utekelezaji unaosababishwa na idadi ndogo ya mabalozi pia
ulidokezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula mapema mwezi huu.
Akizungumzia
suala hilo, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue ambaye alikuwa akijibu
maswali kuhusu vikwazo vitano vya utekelezaji wa agizo hilo la Rais,
alisema suala hilo linaweza kujibiwa vizuri zaidi na Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Lakini msemaji wa wizara hiyo, Mindi Kasiga alisema atumiwe ujumbe wa barua pepe ili ajibu suala hilo.
Ukomo wa madaraka ya mabalozi
Suala
jingine linalozungumziwa ni ukomo wa mabalozi katika mamlaka yao, hasa
pale wanapotakiwa kumuwakilishi Rais wakati hawabebi madaraka hayo ya
mkuu wa nchi. Mara nyingi wakuu wa nchi huona umuhimu zaidi wa kuwa na
mazungumzo baina yao kuliko na mabalozi inapotokea wamekutana kwenye
mikutano ya mikubwa kama ya Jumuiya ya Madola, Umoja wa Mataifa, Sadc na
mingine inayoweka maazimio muhimu kuhusu masuala kama ya mazingira,
afya, na ya kibiashara.
Lakini Balozi Sefue alisema Rais atakuwa
akihudhuria mikutano michache na hivyo uamuzi huo hautaathiri nchi. “Ni
mikutano michache sana ambayo wanahudhuria wakuu wa nchi,” alisema
Balozi Sefue. “Pale ambapo tutajiridhisha kuwa ubalozi hauwezi
kutuwakilisha vizuri, basi tutaruhusu mtu atoke hapa nyumbani. Hiyo
itakuwa ni baada ya kujua ni nani atakayekwenda na atakwenda kufanya
nini,” alisema Balozi Sefue.
Kwa uzoefu wake, alisema hata
viongozi watakaopewa ruhusa hawatakuwa na misafara mirefu kama
ilivyokuwa awali kwa kuwa wapo baadhi yao ambao wanakuwa hawafanyi
chochote huko waendako.
“Nilipokuwa Washington niliwahi kushuhudia.
Kuna msafara ulikuja, mkubwa sana na kwa kipindi chote walichokaa pale,
wapo baadhi hawakupata nafasi ya kufanya chochote. Hili nalo ni miongoni
mwa mambo yatakayozingatiwa katika vibali vitakavyokuwa vinatolewa kwa
wale watakaokidhi masharti,” alisisitiza.
Kuhusu ukubwa wa ujumbe
ambao kiongozi anaruhusiwa kuambatana nao aendapo nje ya nchi, msemaji
wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mindi Kasiga amewahi kufafanua kuwa, kwa
mujibu wa itifaki, kila mmoja ana maelekezo yake.
“Msafara wa Rais
hauwezi kulingana na wa makamu wake, Waziri Mkuu au waziri wa kawaida
ambao pia hutofautiana na makatibu wakuu au wakuu wengine wa idara na
vitengo vya Serikali,” alisema Kasiga wakati akitoa ufafanuzi juu ya
gharama za safari za nje wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Uwakilishi wa mamlaka ya Rais
Mbali
na vikwazo hivyo, suala jingine ni mabalozi kubeba majukumu ya Rais
kwenye mikutano ya nje jambo ambalo wakosoaji wanasema litawawia vigumu
hasa watakapotakiwa kufanya uamuzi kwa madaraka ya mkuu wa nchi.
Lakini
Balozi Sefue alisema mabalozi watakaotumwa kwenye mikutano hiyo
watabeba kofia hiyo ya mkuu wa nchi na taarifa itakayotumwa nchini
itakuwa na uzito unaostahili hivyo suala hilo halitaathiri ushiriki wa
nchi.
Mabalozi kutokuwa na utaalamu
Uwezo wa mabalozi
kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya kitaalamu pia ni moja ya mambo
yanayoonekana kuwa kikwazo kwa agizo la Rais Magufuli kuzuia safari za
nje.
Lakini Balozi Sefue alisema matukio yanayohusu masuala ya
kitaalamu kama kilimo, mazingira, afya, madini na mawasiliano ambayo
yanahitaji watendaji waliobobea kwenye fani hizo, yatawekewa utaratibu
licha ya kuwa changamoto kwa mabalozi.
“Kila ubalozi una wataalamu wa
masuala mbalimbali ambao wanaweza kutoa mchango unaostahili kwa lolote
linaloweza kuhitajika,” alisema.
“Si rahisi kukosa mtu mwenye uwezo
wa kumsaidia balozi kutekeleza majukumu yake kiasi cha kuhitaji mtu
mwingine kutoka nyumbani. Lakini likijitokeza hilo, tutatuma
mwakilishi.”
Akizungumzia suala hilo, Balozi Mulamula alisema mapema
mwezi huu kuwa utekelezaji huo utachukua muda kidogo kutokana na balozi
nyingi kukosa fedha na watalaamu.
Suala la fedha kwenye balozi za
Tanzania limekuwa kilio kikubwa kila wakati wa Bunge la Bajeti na mwaka
huu suala hilo liliibuka kwenye hotuba ya kambi ya upinzani iliyosema
kiasi cha Sh30 bilioni ziloizotengwa kwa wizara hiyo hazikutosha
kuwawezesha mabalozi kufanya kazi yao kwa ufanisi.
Suala la weledi
pia lilizungumzwa kwenye hotuba ya kambi ya upinzani ya mwaka 2014/15
ikisema uteuzi holela wa mabalozi usiozingatia sifa, unalikosesha Taifa
fursa nyingi za kiuchumi kwa kuwa wengi hawana ufahamu wa fursa zilizoko
kwenye nchi wanazokwenda.
Lakini mapema mwezi huu, Balozi Mulamula
alisema suala hilo sasa litaangaliwa kwa jicho la karibu zaidi, hasa
uteuzi wa mabalozi.
Alisema watatoa mwongozo ambao utawataka
wawakilishi hao wasibweteke katika utendaji wao kwa kuwa kuna mpango wa
kuanzisha utaratibu wa kupima matokeo ya utendaji wao kwa kila baada ya
kipindi kitakachoelekezwa.
“Kwa sasa tutakuwa tunawapima mabalozi wetu kwa malengo tuliyokubaliana nao ambayo yanaweza kuwa ya mwaka au zaidi.
Tutakuwa tunamuuliza balozi umeweza kuleta watalii au kuwahamasisha wawekezaji wangapi nchini?” alisema.
“Hii ni kwa sababu zamani tulikuwa tunakwenda kienyeji lakini kwa sasa hapa kazi tu.”
Kikwazo
kingine kinachoonekana kwenye utekelezaji wa agizo hilo ni kukosekana
kwa mazungumzo endelevu iwapo suala moja litawakilishwa na watu wawili
tofauti kwenye mikutano miwili tofauti.
“Mfano iwapo kutakuwa na
mkutano wa suala fulani la Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Kenya, kwa
agizo hilo la Rais, atakayewakilisha ni balozi wa Tanzania nchini
Kenya,” alisema mkosoaji huyo na kuongeza:
“Iwapo suala hilo
litaendelezwa kwenye mkutano mwingine wa jumuiya nchini Uganda, ni
dhahiri atawakilisha balozi wa Tanzania nchini humo ambaye hakuwapo
kwenye mkutano wa Kenya. Kwa hiyo kutakuwa na upungufu.”
Balozi
Sefue hakutaka kufafanua kuhusu hoja hiyo na badala yake akaielekeza kwa
Wizara ya Mambo ya Nje, ambayo alisema ina nafasi nzuri zaidi ya
kulizungumzia.
During its two year run, the project will award approximately 100 major reporting grants and provide mentoring to support the best ideas for stories on development issues. Journalists who produce the best stories published or broadcasted in media that reach African audiences, will win a major international reporting trip. During its two year run, the project will award approximately 100 major reporting grants and provide mentoring to support the best ideas for stories on development issues. Journalists who produce the best stories published or broadcasted in media that reach African audiences, will win a major international reporting trip
Loading...
Home
» JOHN POMBE MAGUFULI
» NEWS
» POLITICS
» Vikwazo Vitano Vyatajwa Kwenye Agizo la Rais Magufuli Kufuta Safari za Nje
Post a Comment